Breaking


Ijumaa, 6 Februari 2026

WAZIRI WA FEDHA ASIFU MICHANGO YA BUNGE KUBORESHA MWONGOZO WA MPANGO NA BAJETI 2026/27–2028/29



Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amewashukuru Wabunge pamoja na wajumbe wa Kamati ya Mipango kwa maoni na ushauri waliotoa, uliosaidia kuboresha Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/27 hadi 2028/29.


Akihitimisha mjadala wa mapendekezo hayo bungeni jijini Dodoma, Mhe. Balozi Omar alisema michango ya Wabunge imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mwongozo huo, hususan katika maeneo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani, fursa za ukopaji kwa Serikali, mwenendo wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, utekelezaji wa sera ya fedha pamoja na maboresho ya maelekezo yaliyomo katika mwongozo huo.


Alifafanua kuwa katika wasilisho lake la tarehe 02 Februari 2026, alieleza kwa kina mwelekeo wa hali ya uchumi wa nchi, utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25, pamoja na vipaumbele vya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha 2026/27 hadi 2028/29. Aidha, alisisitiza maelekezo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa na maafisa masuuli katika kuandaa, kutekeleza, kufuatilia, kutathmini na kutoa taarifa za utekelezaji wa bajeti.


Mhe. Balozi Omar aliongeza kuwa Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti unaakisi jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuboresha maisha ya Watanzania. Alisema jitihada hizo zinalenga kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ili kuvutia sekta binafsi, kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii, kuongeza tija katika sekta za uzalishaji pamoja na kudumisha amani, usalama, utawala bora na mshikamano wa kitaifa.


Katika hatua nyingine, Waziri huyo aliwapongeza wafanyabiashara na wawekezaji kwa mchango wao katika ulipaji wa kodi, uzalishaji wa ajira, ushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii. Vilevile, aliwashukuru wananchi kwa kuendelea kuitikia wito wa kulipa kodi kwa hiari, akisisitiza kuwa mchango huo ni nguzo muhimu katika maendeleo endelevu ya Taifa.


Hakuna maoni: