Breaking


Jumatano, 8 Aprili 2026

DALADALA HATARINI KUSIMAMA DAR NA MWANZA KUTOKANA NA HASARA YA MAFUTA


Katika mkutano wa wadau wa usafirishaji ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra) jijini Dar es Salaam, Umoja wa Wasafirishaji Abiria wa Dar es Salaam na Mwanza umeeleza uwezekano wa kusitisha huduma kutokana na changamoto za uendeshaji. Wadau hao wamewasilisha maoni yao wakieleza kuwa hali ya biashara imekuwa ngumu kufuatia kupanda kwa gharama za mafuta.


Wamesema tangu ongezeko la bei ya mafuta lililotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) Aprili Mosi, 2026, daladala nyingi zimekuwa zikijiendesha kwa hasara kubwa, hali inayotishia upatikanaji wa huduma kwa wananchi. Mwenyekiti wa Uwadar, Jafar Kismat, alieleza kuwa licha ya changamoto hizo, hawataki kufikia hatua ya kugoma kama ilivyowahi kujitokeza katika baadhi ya mikoa mingine.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wasafirishaji Mkoa wa Mwanza, Yusuph Lupilia, alilalamikia pia ushindani kutoka kwa bajaji zinazofanya kazi kama daladala, akisisitiza haja ya kurekebisha nauli. Alipendekeza nauli ya safari za kilomita sifuri hadi 10 iongezwe kutoka Sh600 hadi Sh800 ili kusaidia waendeshaji kumudu gharama na kuendelea kutoa huduma bila usumbufu.


Hakuna maoni: