Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, ameweka wazi msimamo wa klabu kuhusu sakata la mchezaji Mohammed Damaro, akisema licha ya kupokea hukumu iliyotolewa, bado haijajibu hoja zao za msingi.
Ameeleza kuwa Simba tayari imewasilisha maombi ya mapitio ya uamuzi huo, na endapo haitapata haki inayostahili, ipo tayari kupeleka suala hilo katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) pamoja na kuifikisha FIFA ili kufanyiwa uchunguzi wa kina zaidi.
Akizungumzia masuala ya kikosi, Magori amefafanua kuwa Inno Loemba ni mchezaji halali wa Simba aliyepatikana kupitia mchakato wa scouting na kukamilishiwa usajili wake kwa kufuata taratibu zote, ikiwemo malipo yaliyofanywa na mdhamini Jayrutty.
Amebainisha kuwa kutocheza kwa Loemba dhidi ya Azam kulitokana na kurejea kutoka majeruhi, hivyo benchi la ufundi kuona si sahihi kumtumia mara moja katika mechi yenye ushindani mkubwa.
Aidha, amekanusha taarifa za Elia Mpanzu kugoma kucheza, akieleza kuwa alikuwa anaumwa lakini tayari amesafiri kwenda Arusha na huenda akacheza dhidi ya TRA iwapo afya yake itaimarika.
Katika upande wa maendeleo ya klabu, Magori ameeleza kuwa mwekezaji Mohammed Dewji ameomba kujenga uwanja katika eneo la Bunju, huku suala hilo likiwa bado linajadiliwa na Bodi ya Wadhamini kabla ya kupelekwa rasmi kwa Bodi ya Wakurugenzi.
Ameongeza kuwa kampuni ya Jayrutty inaendelea kuwa mdau muhimu kwa kuchangia fedha za ujenzi wa uwanja kila mwaka, na klabu inapanga kukutana nao kujadili mipango ya baadaye.
Kuhusu malalamiko ya waamuzi, amesema hawezi kulizungumzia moja kwa moja kutokana na kanuni, lakini amewahakikishia mashabiki kuwa hatua zinaendelea kuchukuliwa huku akiwataka kuwa watulivu.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni