Breaking


Jumapili, 26 Aprili 2026

MAPENDEKEZO YA THTU KWA SERIKALI KUHUSU KODI, UTAWALA NA UCHUMI WA UBUNIFU


CHAMA cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) kimewasilisha serikalini mapendekezo ya kina yanayolenga kuimarisha mfumo wa kodi, utawala bora pamoja na matumizi ya utafiti na ubunifu kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa taifa, ikiwa ni sehemu ya kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mapendekezo hayo yamewasilishwa kupitia maandiko matatu ya kitaalamu yanayogusa nyanja za uchumi, siasa na sheria pamoja na utafiti na mapato, yakilenga kutoa suluhisho la changamoto za msingi zinazoikabili nchi katika ukusanyaji wa mapato, usimamizi wa rasilimali na matumizi ya maarifa katika maendeleo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa THTU Taifa, Dkt. Paul Loisulie, lengo la maandiko hayo ni kuishauri serikali kuchukua hatua za kimkakati zitakazoongeza mapato ya ndani bila kuongeza mzigo kwa wafanyakazi, huku ikiimarisha misingi ya utawala bora na kuchochea uchumi unaotegemea maarifa.


Amesema katika andiko la kodi na uchumi, chama hicho kimebainisha kuwa uwiano wa mapato ya kodi dhidi ya Pato la Taifa bado ni mdogo, ukiwa kati ya asilimia 11 hadi 13, chini ya kiwango kinachopendekezwa kwa nchi zinazoendelea.

“Tunashauri kupanua wigo wa kodi kwa kujumuisha sekta zisizo rasmi na uchumi wa kidijitali, badala ya kuongeza viwango vya kodi kwa wafanyakazi,” alisema Dk. Loisulie.

Aidha, THTU imependekeza kuanzishwa kwa kodi ya huduma za kidijitali, kuimarisha usimamizi wa kodi kwa kutumia teknolojia, pamoja na kupunguza mzigo kwa wafanyakazi wa kipato cha chini ili kujenga mfumo wa kodi wenye usawa.

Katika andiko la siasa na sheria, chama hicho kimeeleza kuwa mafanikio ya Dira 2050 yanategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa utawala bora, unaojumuisha uwajibikaji, uwazi, ushiriki wa wananchi na ulinzi wa haki za binadamu.

Hata hivyo, THTU imeeleza kuwepo kwa changamoto ya utekelezaji wa sheria, ambapo pamoja na uwepo wa mfumo mzuri wa kikatiba na kisheria, bado kuna mapungufu katika utekelezaji wake kwa vitendo, hali inayoweza kudhoofisha maendeleo ya taifa.

Katika andiko la utafiti na mapato, THTU imebainisha kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya tafiti na ubunifu, lakini matokeo yake hayatumiki kikamilifu kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Chama hicho kimeeleza kuwa tafiti nyingi huishia katika machapisho ya kitaaluma bila kubadilishwa kuwa bidhaa, huduma au ajira, kutokana na ukosefu wa mfumo madhubuti wa kuunganisha utafiti na soko.

Kutokana na hali hiyo, THTU imependekeza kuanzishwa kwa mfumo wa kitaifa unaounganisha utafiti, ubunifu na biashara, kuongeza uwekezaji katika utafiti na maendeleo, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, vyuo vikuu na sekta binafsi

Hakuna maoni: