WAKALA wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya mafuta, umeanzisha mfumo wa kisasa wa Supervisory Control and Data Acquisition (SCADA) unaolenga kudhibiti upotevu wa mafuta kutoka melini hadi kwenye maghala ya kuhifadhi.
Haya yameelezwa na Mkaguzi wa Mafuta wa PBPA, Issa Khamis Mwitazy wakati akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, katika Maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
Amesema Mfumo huo unasoma na kufuatilia kwa wakati halisi ujazo wa mafuta kupitia mita za serikali zilizopo katika bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, pamoja na kusoma kiwango cha mafuta kilichopo kwenye maghala ya wateja.
“Mfumo wa SCADA una uwezo wa kulinganisha ujazo wa mafuta unaopokelewa kutoka melini na yale yaliyohifadhiwa maghala, hatua inayorahisisha kubaini tofauti yoyote inayoweza kuashiria uvujaji au upotevu.”
“Endapo kutakuwa na tofauti ya ujazo kati ya mita za bandarini na mafuta yaliyopo kwenye maghala, mfumo unatoa taarifa mara moja na hivyo kurahisisha kuchukua hatua stahiki.” Amesema Mwitazy
Aidha, Mwitazy amesema mfumo huo pia umeongeza uwazi na udhibiti katika sekta ya mafuta kwa kusaidia kuzuia uchepushaji wa mafuta kutoka ghala moja kwenda jingine kinyume na utaratibu uliopangwa.
“Kutokana na ufanisi wa mfumo wa SCADA na utaratibu wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja umeanza kuvutia wadau wa kimataifa, ambapo nchi jirani zikiwemo Zambia na Malawi zimefika nchini kujifunza namna Tanzania inavyosimamia uagizaji wa mafuta kwa pamoja na kudhibiti upotevu wake.”Ameongeza Mwitazy
Naye Meneja wa Sheria wa PBPA, Lilian Rwegumbura amesema wametumia Wiki ya Nishati kutoa elimu kwa Wabunge kuhusu utaratibu wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja, unaohusisha kuagiza mafuta kwa mpango wa miezi miwili mbele hatua ambayo imesaidia nchi kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni