Breaking


Jumapili, 12 Aprili 2026

MITINDO NI UTAMBULISHO: MIRIAM ODEMBA AIPIGANIA TANZANIA KIMATAIFA

Mwanamitindo nguli Mtanzania Miriam Odemba ametoa wito kwa Serikali kuongeza nguvu katika kuunga mkono tasnia ya mitindo akisisitiza kuwa sekta hiyo ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi, hususan kupitia utalii na ajira. 

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya ‘Muda Tanzanite Gala’, Odemba alieleza kuwa wanamitindo wengi wa Kitanzania wanapata fursa za kwenda nje ya nchi na hivyo kuwa mabalozi wa utamaduni wa Tanzania kimataifa. 

Alisisitiza kuwa mafanikio ya tasnia hiyo yanahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya wadau na Serikali ili kuifikisha mbali zaidi.


Aidha, Odemba alibainisha kuwa mitindo imekuwa zaidi ya mavazi, akieleza kuwa ni njia muhimu ya kujieleza, kujitambulisha na kuonesha utamaduni wa taifa.

 Alitoa hamasa kwa wanamitindo chipukizi na waliobobea kuendelea kujiamini, kufanya kazi kwa bidii na kushikamana ili kuendeleza tasnia hiyo. 

Kwa mujibu wake, mshikamano na juhudi za pamoja zinaweza kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha mitindo barani Afrika na duniani kwa ujumla.


Kwa upande wa washiriki wa hafla hiyo, wengi walikubaliana na kauli ya Odemba wakisisitiza umuhimu wa kuwekeza zaidi katika mafunzo, miundombinu na majukwaa ya kimataifa yatakayowapa nafasi wanamitindo wa ndani kung’ara zaidi. 

Tukio la ‘Muda Tanzanite Gala’ limeonekana kuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji, kuunganisha wadau na kuhamasisha ukuaji wa tasnia ya mitindo nchini, huku likitoa matumaini mapya kwa kizazi kijacho cha wanamitindo Tanzania.


Hakuna maoni: