Breaking


Jumapili, 12 Aprili 2026

TASAC NA NIC ZATOA ELIMU ZA BIMA NA USALAMA MAJINI KWA WADAU WA USAFIRI MAJINI MKOANI KAGERA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Shirika la Bima la Taifa (NIC), wametoa elimu ya bima na usalama majini kwa wadau wa usafiri majini mkoani Kagera, ikiwa ni jitihada za kupunguza ajali na kuongeza ulinzi wa maisha na mali katika maeneo ya Ziwa Victoria.

Akizungumza wakati wa kampeni hiyo, iliyofanyika katika wilaya za Bukoba, Karagwe na Muleba, Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Kagera, Nahodha Mzee Mvihanga, amesema kuwa elimu ya usalama ni msingi muhimu wa kuzuia ajali majini na kusisitiza kuwa abiria wote wanapaswa kuvaa majaketi okozi muda wote wanapokuwa safarini, akionya kuwa ni hatari na kinyume cha taratibu kupanda chombo bila vifaa hivyo muhimu vya kuokoa maisha.

Katika zoezi hilo, TASAC ilitoa mafunzo ya vitendo kuhusu matumizi sahihi ya majaketi okozi, yakilenga kuwawezesha abiria kuelewa namna ya kujikinga wanapokumbana na dharura.

Kwa upande wake, Afisa Bima wa NIC Mkoa wa Kagera, Bw. Alfred Bwojo, alieleza kuwa bima ni nyenzo muhimu ya kuwasaidia wananchi kukabiliana na athari za majanga yasiyotarajiwa. Alibainisha kuwa sekta ya usafiri majini inakabiliwa na hatari mbalimbali, hivyo ni muhimu kwa wamiliki wa vyombo, wasafirishaji na wafanyabiashara kuchangamkia huduma za bima ili kujihakikishia ulinzi.

Aidha, Mkuu wa Kikosi cha Polisi Wanamaji Mkoa wa Kagera, Mrakibu wa Polisi Juma Mbungu amesema kuwa elimu ya usalama ni muhimu kwa abiria na waendeshaji wa vyombo vya usafiri majini na kusisitiza kuwa elimu hiyo itawasaidia abiria kuwa na uelewa wa mbinu sahihi za uokoaji pamoja na namna ya kujilinda wanapokumbana na hatari majini.

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano kwa Umma wa TASAC, Bw. Saidi Mkabakuli amesema kuwa TASAC itaendelea kutoa elimu kwa umma ili kuhamasisha uzingatiaji wa kanuni za usalama majini na kupunguza ajali zinazoweza kuzuilika.

Wadau walioshiriki katika zoezi hilo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakisema imewaongezea uelewa kuhusu umuhimu wa kuchukua tahadhari na kufuata taratibu za usalama.

Hakuna maoni: