Msanii wa muziki D4vd amekamatwa na polisi wa Los Angeles Police Department kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya msichana mwenye umri wa miaka 14 aitwaye Celeste Rivas, tukio lililozua mshtuko mkubwa kwa mashabiki na jamii kwa ujumla.
Kwa mujibu wa taarifa za polisi, msanii huyo anayejulikana pia kama David Anthony Burke alitiwa mbaroni nyumbani kwake jijini Los Angeles na kwa sasa anashikiliwa bila dhamana huku uchunguzi ukiendelea.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Kaunti ya Los Angeles imethibitisha kuwa jalada la kesi hiyo litawasilishwa katika kitengo cha makosa makubwa (Major Crimes Division) ili kupitia ushahidi na kubaini iwapo kuna msingi wa kufungua mashtaka rasmi dhidi yake.
Kukamatwa kwa D4vd kunakuja zaidi ya miezi saba tangu kupatikana kwa mwili wa Celeste ndani ya gari lake aina ya Tesla mnamo Septemba 2025 katika eneo la Hollywood Hills, ambapo ulikutwa ukiwa umeanza kuoza.
Wakati tukio hilo linatokea, msanii huyo alikuwa katikati ya ziara ya muziki kabla ya kusitisha maonesho yake ghafla na kutoweka hadharani, hali iliyoongeza mashaka miongoni mwa wachunguzi.
Uchunguzi unaonyesha kuwa tangu awali polisi walikuwa wakimchukulia kama mtuhumiwa mkuu, huku ushahidi ukiwasilishwa mbele ya jopo la majaji (grand jury) mwezi Novemba chini ya mwendesha mashtaka Beth Silverman.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa D4vd alikuwa na uhusiano na marehemu Celeste, ambaye aliripotiwa kupotea tangu Aprili 2024 kabla ya mwili wake kugunduliwa kufuatia gari lake kutelekezwa na baadaye kuvutwa hadi kituo cha polisi kutokana na harufu iliyozua taharuki.
Polisi pia wanachunguza safari ya usiku aliyofanya msanii huyo kuelekea Santa Barbara wakihisi huenda ina uhusiano na tukio hilo.
Wakati huo huo, mazishi ya Celeste yalifanyika Oktoba 6 katika Queen of Heaven Cemetery & Mortuary huku familia na marafiki wakitoa heshima za mwisho, na jamii ikiendelea kusubiri hatua zaidi za kisheria zitakazochukuliwa kadri uchunguzi unavyoendelea.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni