Bohari ya Dawa (MSD) imeongeza juhudi katika kusambaza dawa za kukabiliana na sumu ya nyoka kufuatia kuongezeka kwa matukio ya wananchi kung’atwa na nyoka katika baadhi ya mikoa nchini, ikiwemo Tabora, Kigoma na Katavi. Hatua hiyo inalenga kupunguza madhara na kuokoa maisha ya wananchi wanaokumbwa na tatizo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa, licha ya kukosekana kwa takwimu rasmi zinazoonesha ukubwa wa changamoto hiyo kwa kila mkoa, mahitaji ya dawa hizo yamekuwa yakiongezeka katika vituo vya afya. Ongezeko hilo linaashiria kuongezeka kwa matukio ya kung’atwa na nyoka katika jamii, hususan maeneo ya vijijini na yenye shughuli nyingi za kilimo.
Akizungumza jijini Dodoma katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari, Meneja wa MSD Kanda ya Tabora, Rashid Omary, amesema taasisi hiyo imechukua hatua za haraka kuhakikisha dawa za kutibu sumu ya nyoka zinapatikana kwa wakati katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.
Amefafanua kuwa katika kipindi cha miezi tisa kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026, MSD Kanda ya Tabora imesambaza jumla ya dozi 202 za dawa za kupambana na sumu ya nyoka kwa vituo vya afya vilivyowasilisha maombi rasmi.
“Usambazaji huu unazingatia mahitaji halisi kutoka vituo vya afya, jambo linaloonesha wazi kuwa matukio ya kung’atwa na nyoka bado ni changamoto inayohitaji uangalizi wa karibu,” amesema Omary.
MSD imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha mfumo wa usambazaji wa dawa hizo muhimu, sambamba na kushirikiana na wadau wa sekta ya afya ili kuhakikisha upatikanaji wake unaimarika zaidi, hasa katika maeneo yaliyo hatarini.
Hatua hizi zinatarajiwa kusaidia kupunguza madhara makubwa ya kiafya pamoja na vifo vinavyoweza kusababishwa na sumu ya nyoka, huku juhudi za utoaji elimu kwa jamii kuhusu tahadhari zikiendelea kupewa kipaumbele.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni