Wakala wa Nishati Vijijini- REA, umetangaza mafanikio makubwa ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza nishati vijijini, huku ukieleza kuwa vijiji vyote nchini tayari vimefikishiwa umeme na sasa nguvu kubwa imeelekezwa katika vitongoji.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini REA, Mhandisi Jones Olotu, amesema safari ya kusambaza umeme ilianza mwaka 2008 kwa bajeti ndogo lakini imezaa matokeo makubwa.
Miradi ya REA I, II na III imefanikisha kufikisha umeme katika vijiji vyote, huku hatua ya sasa ikilenga vitongoji 64,359 ambapo hadi sasa zaidi ya vitongoji 50,447 vimefikiwa au vina miradi inayoendelea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala REA, Mhandisi Advera Mwijage, amesema juhudi hizo zinaongezewa nguvu na miradi ya gridi ndogo zaidi ya 70 inayotumia nishati ya jua na maji.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano REA, Martha Chassama, amesema mafanikio hayo yamechangiwa na ushirikiano kati ya REA, viongozi wa serikali za mitaa na wananchi.
Naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania-TEF, Deodatus Balile, ameipongeza REA akisema ni taasisi inayotekeleza mipango yake kwa ufanisi mkubwa ikilinganisha na nyingine za umma.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni