Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha huduma za wagonjwa wa dharura na mahututi katika Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, hatua inayoongeza ujuzi kwa watumishi wa afya na kuboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka.
Wataalamu wa afya wa Hospitali ya Wilaya ya Kakonko wamepongeza juhudi hizo, wakieleza kuwa mafunzo na usimamizi shirikishi unaotolewa na wataalamu kutoka Wizara ya Afya umeongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za dharura na maafa.
Akizungumza Aprili 18, 2026, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Kakonko, Dkt. Nyetera Nyangi, alisema mafunzo hayo yamekuwa na mchango mkubwa kwenye kuboresha huduma kwa wagonjwa wa dharura, hususan waathirika wa ajali za barabarani, wenye matatizo ya mfumo wa hewa, magonjwa ya moyo pamoja na waliopata kiharusi cha ghafla.
Amesema kuwa uboreshaji huo umechangiwa na upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa na vya kutosha, vinavyorahisisha utoaji wa huduma kwa wakati.
Aidha, Dkt. Nyangi amebainisha kuwa huduma za dharura zilianza rasmi wilayani humo mwaka 2024 baada ya Serikali kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo maalum la huduma za dharura (EMD) pamoja na ununuzi wa vifaa tiba, hatua iliyoongeza kiwango cha huduma kwa kiasi kikubwa.
Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha watumishi wa hospitali hiyo kupata mafunzo katika Hospitali ya Bugando kuhusu huduma za dharura (EMD) na wagonjwa mahututi (ICU).
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kakonko, Dkt. Khalid Ukwete, amesema ujio wa wataalamu hao umeimarisha uwezo wa watumishi kwenye matumizi sahihi ya vifaa tiba na mbinu bora za utoaji huduma, sambamba na kusaidia kubaini changamoto zilizopo.
Naye Afisa Tabibu wa hospitali hiyo, Penina Kimei, amesema mafunzo hayo yamewaongezea ujuzi wa uokoaji wa wagonjwa wa dharura, matumizi ya teknolojia za kisasa pamoja na utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa moyo.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni