Tanzania imeendelea kuimarisha diplomasia ya elimu kufuatia ushiriki wake katika ziara ya kikazi jijini Ottawa, Canada, hatua iliyofungua fursa mpya za ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili katika sekta ya elimu.
Katika ziara hiyo iliyoanza Aprili 20 na inatarajiwa kumalizika Aprili 25, 2026, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhamed Musa akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, pamoja na ujumbe wa wataalamu wa elimu, wamekutana na wadau mbalimbali wa elimu kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kujadili fursa zitakazowanufaisha Watanzania.
Ziara hiyo imefanyika kufuatia mwaliko wa Chama cha Vyuo vya Ufundi nchini Canada (Colleges and Institutes Canada – CiCan), ambapo Tanzania ilishiriki katika mkutano mkubwa wa Connections Conference unaowakutanisha viongozi wa vyuo vya ufundi kujadili changamoto za kiuchumi na kijamii zinazoikabili dunia. Kupitia mkutano huo, Tanzania imepata jukwaa la kuonesha vipaumbele vyake na kuanzisha mazungumzo ya awali ya ushirikiano na taasisi mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Mhe. Musa amekutana na uongozi wa vyuo vikuu vya Canada kwa lengo la kupanua ushirikiano katika ngazi ya vyuo vikuu, pamoja na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Maendeleo (IDRC) ili kuimarisha tafiti zitakazosaidia kuelekeza maendeleo ya nchi katika maeneo ya kimkakati.
Katika kuendeleza uhusiano wa kitaaluma, ujumbe wa Tanzania umetembelea Chuo Kikuu cha Ottawa, Chuo Kikuu cha Carleton na Chuo cha Ufundi cha Algonquin, ambako mazungumzo yalijikita katika kubadilishana wataalamu na wanafunzi, pamoja na kujenga uwezo wa walimu na kuboresha mitaala, hasa katika nyanja za ujenzi, ubunifu, sayansi na teknolojia.
Aidha, Waziri huyo amekutana na Mwakilishi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) nchini Canada, ambapo walijadili namna ya kuimarisha programu za maendeleo zinazotekelezwa Tanzania kwa ufadhili wa Serikali ya Canada. Ushirikiano huo unahusisha pia Chuo Kikuu cha Aga Khan Tanzania katika maeneo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni