Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesema kuwa mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) ili kurahisisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini pamoja na kuimarisha mapambano dhidi ya magendo.
Kamishna Mkuu Mwenda ametoa kauli hiyo Aprili 20, 2026, wakati wa kikao kati ya TRA na viongozi wa JWT pamoja na baadhi ya wafanyabiashara wa mafuta ya kula, kilichofanyika katika ofisi za TRA jijini Dar es Salaam.
Aidha, amesisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa biashara zinaendeshwa kwa uwazi na kwa kuzingatia sheria za kodi, hali itakayochochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Mbali na hayo, Kamishna Mkuu amegusia changamoto ya uingizaji wa mafuta kutoka Zanzibar kuja Tanzania Bara, akieleza kuwa serikali kupitia TRA inaifanyia kazi na kwamba ufumbuzi wake utapatikana hivi karibuni ili kuondoa mianya ya ukwepaji kodi na ushindani usio wa haki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JWT Bw. Khamisi Livembe, amesema kuwa wafanyabiashara wako tayari kushirikiana na TRA katika juhudi za kukomesha magendo, akibainisha kuwa vitendo hivyo vinachangia kuvuruga ushindani wa haki katika soko.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Bw. Omar Hussein Mussa, amewasihi wafanyabiashara kuachana na vitendo vya magendo na badala yake kuendesha biashara zao kwa njia halali, akisisitiza umuhimu wa kuchangia kodi kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya maendeleo ya taifa na mustakabali wa Tanzania.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni