Rais wa Marekani, Donald Trump, ameibua taharuki kubwa duniani baada ya kutoa kauli kali akidai kuwa ana uwezo wa “kuifuta kabisa” nchi ya Iran ndani ya usiku mmoja iwapo haitatii masharti ya Marekani.
Kauli hiyo imekuja wakati mvutano mkali ukiendelea kati ya Marekani na Iran, hasa kuhusu kufunguliwa kwa mlango muhimu wa usafirishaji mafuta wa Strait of Hormuz. Trump aliweka wazi kuwa endapo Iran haitafungua njia hiyo kwa wakati alioweka, hatua kali za kijeshi zitachukuliwa mara moja.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, Trump alisisitiza kuwa mashambulizi hayo yatalenga miundombinu muhimu kama vituo vya umeme na madaraja, hatua ambayo imeibua ukosoaji mkubwa kutoka kwa wanasiasa na jumuiya ya kimataifa.
Wakati huo huo, Iran imejibu kwa msimamo mkali, ikionya kuwa itatoa kisasi kikubwa endapo Marekani itatekeleza vitisho hivyo. Hali hii imeongeza hofu ya kuzuka kwa vita kubwa zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Mvutano huu tayari umeanza kuathiri uchumi wa dunia, huku bei za mafuta zikiongezeka na masoko ya fedha kuyumba kutokana na hofu ya vita kuongezeka.
Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanaonya kuwa kauli kama hizi zinaweza kuchochea mgogoro mkubwa zaidi, huku juhudi za kidiplomasia zikiendelea kufanyika ili kuzuia hali isizidi kuwa mbaya.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni