Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, zimeendelea kuimarisha ushirikiano wake wa muda mrefu kupitia shughuli na masuala mbalimbali ikiwemo kutoa misaada kwa wahitaji mbalimbali katika jamii wakiwemo wagonjwa.
Wizara hizo kupitia Klabu zao za michezo zimejenga utaratibu wa kukutana kila mwaka kwenye Bonanza ya michezo, kutembelea na kuwapatia watu wenye uhitaji, mahitaji mbalimbali ikiwemo vyakula, vinywaji, sabuni na mahitaji mengine muhimu, ambapo kwa mwaka huu wametembelea wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, waliopatiwa mahitaji muhimu ikiwemo mafuta ya kupaka sabuni na mahitaji mengine muhimu.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi mahitaji hayo, Mkurugenzi Mwendeshaji na Utumishi Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Bwana Rajabu Weje Yakubu, kwa niaba ya Wizara za Fedha pande zote mbili, alisema kwa mwaka huu walitembelea wodi ya wanawake na Watoto katika hospitali hiyo na kuwapatia mahitaji mbalimbali.
“Mwaka huu tulipanga kutembelea wodi ya kina mama na watoto, ambapo kwenye wodi ya kina mama tumetembelea kina mama wapatao 38 na kwenye wodi ya watoto tumewatembelea watoto 44 wenye umri chini ya miaka mitano” alisema Bw. Yakubu
Akizungungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala, Bw. Simbani Mganga, katika hospitali hiyo, Afisa Utumishi Mwandamizi, Wizara ya Fedha, Bw. Salum Said, alisema kuwa Wizara hizo zitaendelea na utaratibu huo wa kukutana kila mwaka kama sehemu ya kuadhimisha sikukuu ya Pasaka kwakuwa utaratibu huo ni muhimu kwa watumishi wa pande zote mbili na jamii kwa ujumla.
“Ni kawaida yetu kwa maana ya Wizara ya Fedha Tanzania Bara na Visiwani katika kuadhimisha sherehe za Sikuku ya Pasaka huwa tuna kawaida kutembeleana kwa kila mwaka, ambapo mwaka jana tulikwenda Zanzibar na mwaka huu wao wametutembelea ili kudumisha uhusiano wa kikazi yaliyodumu kwa muda mrefu” Alisema Bw. Said.
Baada ya tukio hilo, watumishi hao wan Wizara ya Fedha Tanzania na Zanzibar, walaiokutana kwa bonanza la michezo mbalimbali, waliagana katika Ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Gerwill jijini Dodoma.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni