Hospitali ya Taifa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili imezindua gari maalum la kisasa la upasuaji kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za kibingwa na kuwafikia wananchi wanaoishi maeneo mbalimbali nchini kupitia huduma za mkoba.
Uzinduzi wa gari hilo umefanyika Mei 20, 2026 jijini Dar es Salaam, ambapo Naibu Waziri wa Afya, Florence Samizi, akimwakilisha Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa, amesema hatua hiyo ni mafanikio makubwa katika juhudi za Serikali kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, hasa wale wa maeneo ya vijijini na yenye changamoto za miundombinu.
Amesema wananchi wengi wamekuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibingwa za upasuaji, hali inayosababisha gharama kubwa pamoja na ucheleweshaji wa matibabu. Kupatikana kwa gari hilo kutasaidia kuwafikia wananchi kwa haraka zaidi na kupunguza changamoto hizo.
Dkt. Samizi pia ameipongeza Sokus Kova Foundation kwa kuwezesha upatikanaji wa gari hilo kutoka nchini China, akieleza kuwa msaada huo utaongeza uwezo wa Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini.
“Sasa huduma za upasuaji zinaweza kutolewa mahali popote bila wananchi kulazimika kufika hospitalini. Hii ni hatua kubwa katika kuimarisha huduma za afya nchini,” amesema Dkt. Samizi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Delilah Kimambo, amesema gari hilo limefungwa teknolojia ya kisasa pamoja na vifaa maalum vya upasuaji vitakavyowezesha utoaji wa huduma mbalimbali za kibingwa.
Amefafanua kuwa huduma zitakazotolewa kupitia gari hilo ni pamoja na operesheni za dharura, uchunguzi wa awali wa wagonjwa pamoja na huduma nyingine za kibingwa zinazohitaji vifaa vya kisasa.
Dkt. Kimambo amesema gari hilo litakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa maeneo ya mbali ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa huduma za kibingwa kutokana na changamoto za umbali, gharama za usafiri na uhaba wa huduma maalum za afya.
Gari hilo ambalo lina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja ni la kwanza la aina yake nchini Tanzania, na linatarajiwa kusaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma za kibingwa katika maeneo yenye uhaba wa miundombinu ya afya.
Uzinduzi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuendelea kuboresha sekta ya afya kwa kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi, kupunguza gharama za matibabu na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni