Hatua hiyo imekuja kufuatia juhudi za Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Ghana kufuatilia usalama wa raia wake wanaoishi Afrika Kusini, wakati hali ya taharuki ikiongezeka katika baadhi ya maeneo yanayoripotiwa kushuhudia vitisho na manyanyaso dhidi ya wageni.
Tangu mwezi Aprili mwaka huu, wahamiaji kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wamekuwa wakikumbana na mazingira magumu, yakiwemo vitisho, mashambulizi ya maneno na hofu ya usalama wao kutokana na kampeni zinazopinga uwepo wa wageni nchini Afrika Kusini.
Moja ya kampeni zinazotajwa kuendelea kushika kasi ni ya kundi la “March and March Movement”, ambalo limekuwa likiwatuhumu wahamiaji kwa madai ya kuchukua nafasi za ajira za wananchi wa Afrika Kusini pamoja na kuhusishwa na vitendo vya uhalifu.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kijamii na haki za binadamu wameonya kuwa ongezeko la chuki dhidi ya wahamiaji linaweza kuathiri mshikamano wa bara la Afrika pamoja na usalama wa raia wa mataifa mbalimbali wanaoishi nje ya nchi zao.
Serikali ya Ghana imeendelea kuwahimiza raia wake waliopo Afrika Kusini kufuata sheria za nchi hiyo huku ikiendelea kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha usalama wao unalindwa.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni