Breaking


Jumamosi, 16 Mei 2026

MWENGE WAPITA NYASA, MRADI WA REA WA BILIONI 4 WAZINDULIWA

 


Wananchi wa Kitongoji cha Ndecha Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wameanza kushuhudia mwanga wa matumaini baada ya kuzinduliwa rasmi kwa mradi wa REA kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 4.17 wa kusambaza umeme unaotekelezwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), mradi ambao unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa eneo hilo.

Mradi huo umezinduliwa leo tarehe 16 Mei, 2026 na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, ambaye amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma bora za nishati ili kuboresha maisha yao na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Halikadhalika  Mwang'onda  amewataka wananchi kutumia nafasi hiyo ya mradi kulipa shilingi 27,000 tu ili waweze kuwekewa umeme huo. 

Kwa upande wake, Msimamizi wa Miradi ya REA Mkoa wa Ruvuma, Mha. Hamisi  Mrope, amesema mradi wa kusambaza umeme vijijini (REDP2C) katika Wilaya ya Nyasa unalenga kufikisha huduma ya umeme katika vitongoji vyote ili kuinua maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, Mha. Mrope amesema mradi huo ulianza rasmi tarehe 16 Novemba 2023 na unatarajiwa kukamilika  ifikapo mwezi Oktoba, 2026, huku ukihusisha vitongoji 30, mashine umba 30 pamoja na wateja 1,247 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 4.17.

Katika Kitongoji cha Ndecha pekee, mradi umehusisha ujenzi wa kilomita 8.43 za njia ya umeme, ufungaji wa mashine umba mbili pamoja na kuunganisha wateja 94 kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 307.6. Hadi sasa, miundombinu imekamilika kwa asilimia 100 huku wananchi 56 tayari wakiwa wameunganishiwa huduma ya umeme kwa gharama nafuu ya shilingi 27,000 kwa kila mteja.

Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi mzawa MF Electrical Engineering Ltd chini ya usimamizi wa TANESCO.

Naye, Mbunge wa jimbo  la Nyasa John Nchimbi amesema miradi ya REA imesaidia kwa sasa vijiji vyote 84 vya wilaya Nyasa kupata huduma ya umeme huku Tanzana ikijivunia kuwa ya pili Afrika Mashariki kwa kusambaza umeme.

Kwa upande wake, Mkandarasi wa mradi huo MF Electrical Engineering Ltd mhandisi Mussa David amesema mradi huo kwa kitongoji cha Ndecha 1 wameshafikisha umeme na wameshawasha nyumba 56.

Wananchi wa Ndecha wameeleza furaha yao kutokana na ujio wa umeme ambapo mwenyekiti wa kijiji cha Linda Antony Nkoma amesema  sasa wataweza kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa ufanisi zaidi tofauti na zamani walipotegemea taa za vibatari na vyanzo vya nishati visivyo salama.

Hakuna maoni: