Breaking


Alhamisi, 21 Mei 2026

NEMC HUPOKEA MALALAMIKO 713 YA KELELE KWA MWEZI MMOJA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira-NEMC, limeendelea kuimarisha usimamizi wa uchafuzi wa kelele nchini baada ya kubainika kuwa linapokea wastani wa malalamiko 23 kwa siku, sawa na takribani malalamiko 713 kwa mwezi mmoja.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Utekelezaji na Uzingatiaji wa Mazingira wa NEMC, Elibarik Majuta, malalamiko mengi yanahusisha matumizi ya sauti kubwa katika maeneo ya biashara, burudani na ibada, hali inayosababisha usumbufu kwa wananchi na kuathiri mazingira ya makazi.

Kutokana na ongezeko la malalamiko hayo, NEMC imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya taasisi na biashara zinazokiuka viwango vya kelele vilivyowekwa na sheria za mazingira.

Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa ni kutoa maonyo, kutoza faini, kusitisha matumizi ya vifaa vya sauti vinavyokiuka masharti pamoja na kufunga kwa muda baadhi ya baa, na  kumbi za starehe zinazoshindwa kuzingatia maelekezo ya udhibiti wa kelele.

Lengo la hatua hizo si kuzuia shughuli za kijamii au kiuchumi, bali kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa kuzingatia haki za wananchi wengine kupata mazingira tulivu na salama.

Wataalamu wa mazingira wanaeleza kuwa kelele zisizodhibitiwa zinaweza kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo msongo wa mawazo, kukosa usingizi, kupungua kwa umakini katika kazi na masomo pamoja na athari nyingine za kiafya, hivyo kufanya udhibiti wake kuwa jambo la msingi kwa ustawi wa jamii. 

Hakuna maoni: