Breaking


Ijumaa, 22 Mei 2026

PROGRAMU YA MAGEUZI YA MAZINGIRA KUZINDULIWA JUNI 5, 2026


Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajiwa kuzindua Programu ya Kitaifa ya Mageuzi ya Kimkakati ya Mazingira Endelevu Tanzania katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yatakayofanyika kitaifa jijini Dodoma Juni 5, 2026.

Akizungumza jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usafi wa mazingira kuelekea siku hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Hamad Yussuf Masauni, amesema programu hiyo inalenga kuifanya Tanzania kuwa mfano wa kimataifa katika uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Masauni amesema mpango huo unatekeleza Dira ya Taifa ya 2050, hususan nguzo ya uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Ameeleza kuwa Serikali inalenga kupanda miti bilioni mbili kila mwaka, kuimarisha biashara ya kaboni, kuanzisha bustani za kijani mijini pamoja na kuongeza matumizi ya nishati safi.


Aidha, amesema programu hiyo inatarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 25,000 ifikapo mwaka 2030 kupitia sekta za taka, misitu, kaboni na nishati safi, hatua inayotarajiwa kuchangia ukuaji wa uchumi wa kijani nchini.

Waziri huyo amebainisha kuwa Tanzania inaendelea kukabiliwa na changamoto za uharibifu wa mazingira, huku takwimu zikionyesha kuwa zaidi ya hekta 469,000 za misitu hupotea kila mwaka kutokana na matumizi makubwa ya kuni na mkaa, kilimo kisicho endelevu pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu.

Kwa upande wa Jiji la Arusha, amesema tafiti zinaonesha kuwa zaidi ya tani 550 za taka ngumu huzalishwa kila siku, ambapo zaidi ya asilimia 60 zina uwezo wa kurejelezwa ikiwa zitasimamiwa vizuri kupitia uchumi rejeshi.


Masauni amesisitiza umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kama njia ya kupunguza ukataji miti, kulinda afya za wananchi na kukabiliana na ongezeko la gesi joto linalochangia mabadiliko ya tabianchi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amesema jamii ina wajibu wa kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi, huku akieleza kuwa jiji hilo linaendelea kuhamasisha wananchi na wanafunzi kushiriki katika shughuli za usafi na uhifadhi wa mazingira.


Hakuna maoni: