Breaking


Jumamosi, 16 Mei 2026

SERIKALI YAFIKISHA UMEME KATIKA MIGODI 289 YA WACHIMBAJI WADOGO HADI MEI 2026.

Naibu Waziri wa Nishati,Salome Makamba,amesema hadi kufikia Mei 2026, jumla ya migodi 289 ya wachimbaji wadogo imepatiwa umeme ikiwemo migodi 18 katika Jimbo la Lupa wilayani Chunya mkoani Mbeya.

Migodi hiyo ni pamoja na Singa, Chokaa Moja, Mapogoro, Godima Beston, Matfra, Mwambe Mlimanjiwa, Mamboleo, Mbiwe na Mwaoga mbili.

Naibu Waziri Salome Salome amesema  hayo Mei 15, 2026 katika Kikao cha 30 cha Mkutano wa tatu wa Bunge la 13 unaoendelea bungeni jijini Dodoma alipokua akijibu swali la Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka aliyehoji mpango wa serikali wa kupeleka umeme kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo.

Aidha amesema Serikali kupitia kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme katika maeneo ya wachimbaji wadogo wa madini, mashamba ya kilimo na viwanda katika mikoa yote nchini ambapo mpango uliopo kwa sasa ni kufikisha umeme katika maeneo 308 ya wachimbaji wadogo ifikapo Juni 2027.

" Serikali kupitia REA itaendelea kupeleka umeme katika migodi midogo midogo iliyosalia ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kuunganisha umeme katika migodi yao," Amesema Salome.

Hakuna maoni: