Breaking


Jumamosi, 16 Mei 2026

TAKUKURU SINGIDA YAREJESHA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 167 ZA MIRADI YA MAENDELEO


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Singida (TAKUKURU) imerejesha serikalini zaidi ya Shilingi milioni 167 zilizobainika kupotea katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani humo.


Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Sosthenes Kibwengo amesema fedha hizo zimerejeshwa kufuatia ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma uliofanyika kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.


Amesema kati ya fedha zilizorejeshwa, zaidi ya Shilingi milioni 56 zilihusishwa na mfumo wa ukusanyaji mapato kwa kutumia mashine za kielektroniki (POS) katika Halmashauri za Manyoni na Iramba, ambapo fedha hizo hazikuwasilishwa benki kwa wakati kama taratibu zinavyoelekeza.


Kibwengo amesema mara baada ya TAKUKURU kuanza uchunguzi, wahusika walirejesha fedha hizo katika akaunti za halmashauri husika huku uchunguzi zaidi ukiendelea ili kubaini wote waliohusika na kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.


Aidha, TAKUKURU imewataka wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma ili kusaidia kulinda rasilimali za serikali na kuhakikisha uwajibikaji unaimarika.

Hakuna maoni: