Breaking


Jumatano, 20 Mei 2026

TANROADS YAJENGA KM 243 ZA BARABARA ZA LAMI NDANI YA MIEZI 10

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania-TANROADS, imeendelea kuimarisha sekta ya miundombinu nchini kwa kufanikisha ujenzi wa barabara na madaraja katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026 chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma leo, Ulega, amesema Serikali imefanikiwa kujenga barabara za kitaifa kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 243.13 pamoja na kufanya ukarabati wa kilometa 94.36 kwa kiwango cha changarawe.

Mtandao wa barabara za kitaifa unaosimamiwa na Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS una jumla ya kilometa 37,734.41 ambapo kilometa 12,225.26 tayari zimejengwa kwa kiwango cha lami.

Amefafanua kuwa wakati Tanzania inapata uhuru mwaka 1961, mtandao wa barabara za lami ulikuwa na urefu wa kilometa 1,360 pekee, huku kuanzia Awamu ya Kwanza hadi ya Tano zikijengwa kilometa 9,369.81. Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kujenga kilometa 1,495.45 za barabara pamoja na madaraja makubwa 18 ndani ya miaka mitano.

Ulega, amesema barabara zinaendelea kuwa mhimili mkuu wa usafiri nchini kutokana na kufika katika maeneo mengi zaidi ikilinganishwa na miundombinu mingine ya usafiri na usafirishaji.

Hakuna maoni: