Breaking


Alhamisi, 21 Mei 2026

TANZANIA YAANZA MAZUNGUMZO NA UONGOZI WA TAMASHA LA FILAMU LA CANNES KUIMARISHA USHIRIKI WA SEKTA YA FILAMU

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Saidi Yakubu, amefanya mazungumzo na viongozi wa Tamasha la Filamu la Cannes nchini Ufaransa kuhusu  kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika tamasha hilo maarufu duniani na kutafuta fursa za ushirikiano zitakazowanufaisha wadau wa tasnia ya filamu nchini.

Katika kikao hicho Balozi Yakubu aliambatana na Bw. Jigar Ganatra, mtayarishaji na mwongozaji wa filamu wa Kitanzania mwenye uzoefu mkubwa wa kimataifa ambapo walikutana  na viongozi waandamizi wa tamasha hilo, akiwemo Bw. François Desrousseaux anayehusika na mahusiano ya kimataifa na Bw. Guillaume Esmiol, Mkurugenzi Mtendaji wa Soko la Filamu la Cannes. 

Mazungumzo hayo yalijikita katika mikakati ya kuongeza ushiriki wa Tanzania katika Tamasha hilo kuanzia mwaka 2027 na  maeneo makuu yaliyojadiliwa ni uanzishwaji wa banda la Tanzania, ushiriki wa watayarishaji na waigizaji wa ndani, fursa za mafunzo kwa vijana, na ushirikiano wa kimataifa katika utengenezaji wa filamu.

“Sekta ya filamu ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, ajira kwa vijana, na utalii hivyo ubalozi utaendelea kushirikiana na wadau wa Ufaransa na Ulaya ili kufungua milango ya uwekezaji katika sekta hiyo” alisema Balozi Yakubu.

Tamasha la Filamu la Cannes ni jukwaa kubwa zaidi duniani linalowakutanisha wadau wa biashara ya filamu kutoka nchi zaidi ya 140 kila mwaka.

Hakuna maoni: