Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027, inatarajiwa kusomwa kesho Bungeni jijini Dodoma, huku Watanzania wakiwa na matarajio makubwa katika bajeti hiyo.
Katika maoni yao baadhi yao wanatamani kuona bajeti kuu ya serikali ikithibiti bei ya mafuta, mfumko wa bei, izuie matumizi holela ya serikali hasa magari.
Leo katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, akielezea mwelekeo wa bajeti kuu ya serikali, amesema itakuwa ni bajeti ya kipekee.
Ni ya kipekee kwa kuwa ni bajeti ya kwanza katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano kuanzia mwaka 2026/2027 hadi 2030/31, na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025-2030.
Dira 2050 ilipozinduliwa na Rais, Dokta Samia Suluhu Hassan, mwezi Julai mwaka 2025, iliweka matumaini makubwa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Taifa na wananchi wake.
Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, mkazo mkubwa utawekwa katika kuendeleza miradi ya kimkakati ya ujenzi wa reli ya kisasa-SGR, ujenzi wa mtandao wa Barabara, kuendelea na uwekezaji katika mtandao wa Taifa wa Maji, miradi ya nishati, na ujenzi wa rasilimali watu na ujuzi.
Mwelekeo wa bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha 2026/2027, serikali inatarajia kutumia zaidi ya shilingi Trilioni-62.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni