Breaking


Jumatano, 10 Juni 2026

PPP HAINA MBADALA KUFIKIA UCHUMI WA DOLA TRILIONI 1

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi-PPP Centre, David Kafulila, amesema Tanzania inahitaji kuongeza kasi ya maendeleo kuliko ilivyofanya Singapore ili kufikia lengo la kuwa na uchumi wa dola trilioni-1 ifikapo mwaka 2050.

Kafulila, ametoa kauli hiyo wakati akieleza ziara ya Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, pamoja na Mhadhara wake Chuo Kikuu cha Dar es salaam-UDSM, ziara ambayo imeibua hamasa miongoni mwa viongozi wa serikali, wanazuoni, wawekezaji na wananchi kuhusu safari ya maendeleo ya Singapore kutoka Taifa la kipato cha chini hadi kuwa miongoni mwa mataifa yenye maisha bora zaidi duniani.

Akinukuu takwimu za IMF za mwaka 2026, Kafulila, amesema Singapore ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani kwa pato la mtu mmoja mmoja, likifikia zaidi ya dola 107,000 kwa mwaka, hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, uchumi wa Singapore bado haujafikia dola trilioni-1, ukiwa na thamani ya takribani dola bilioni-659.

Mwaka 1995 uchumi wa Singapore ulikuwa karibu sawa na wa Tanzania, ukiwa katika kiwango cha dola bilioni-87, jambo linaloonesha kuwa Tanzania inapaswa kuongeza kasi zaidi ya ile iliyotumiwa na Singapore ili kufikia lengo la uchumi wa dola trilioni-1 ifikapo mwaka 2050.

Wakati huo huo, katika ziara yake nchini Tanzania Rais wa Singapore, Tharman, amesisitiza umuhimu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi-PPP, akizitaka serikali za Afrika kuacha kuendesha miradi ambayo inaweza kufanywa kwa ufanisi zaidi na sekta binafsi.

Hakuna maoni: