Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameshiriki kwenye Maadhimisho ya Miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Leo tarehe 12 Juni, 2026, ambapo Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza wakati akimkaribisha Mgeni rasmi, Mhe. Balozi Omar alisema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Benki Kuu huku ikiheshimu uhuru wake wa kisheria na kitaasisi, ili kuhakikisha taasisi hiyo inatekeleza kikamilifu majukumu yake katika kusimamia uthabiti wa uchumi wa nchi.
Alisema ushirikiano uliopo kati ya Serikali na Benki Kuu, hususan katika masuala ya sera za fedha na sera za kibajeti, umechangia kuimarisha uchumi wa Taifa na utaendelea kuimarishwa katika kutekeleza majukumu mapya yanayoendana na mahitaji ya maendeleo ya Tanzania.
Mhe. Balozi Omar alieleza kuwa, ili Taifa lifanikiwe kufikia matarajio yake ya ukuaji wa uchumi na mageuzi ya kiuchumi, ni lazima taasisi muhimu za kiuchumi, ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ziendane na mwelekeo mpya wa maendeleo kwa kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na changamoto na kutumia fursa zinazojitokeza katika mazingira ya uchumi wa kisasa.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni