Breaking


Ijumaa, 12 Juni 2026

TANZANIA YAENDELEA KUIMARISHA NAFASI YAKE KATIKA AJENDA YA WANAWAKE, AMANI NA USALAMA DUNIANI.

Tanzania imeendelea kuimarisha ushiriki wake katika majukwaa ya kimataifa yanayolenga kukuza usawa wa kijinsia, amani na usalama kwa kushiriki katika Mkutano wa Nane wa Ngazi ya Juu wa Mtandao wa Kimataifa wa Nchi zinazotekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama (WPS) uliofanyika jijini Rome, Italia kuanzia Juni 8 hadi 10, 2026.

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Jinsia na Wanawake kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu,ameongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo ulioandaliwa na Sekretarieti ya Mtandao wa Kimataifa wa WPS chini ya UN Women kwa ushirikiano na Italia na Ufilipino, na kuwakutanisha wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 70 kujadili namna ya kuendeleza ajenda ya wanawake katika masuala ya amani na usalama duniani.

Washiriki wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha utekelezaji wa Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama kwa kuweka mikakati inayolenga matokeo ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za amani na usalama zinazoendelea kujitokeza katika maeneo tofauti duniani.

Mkutano huo pia ulijadili haja ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika kuzuia na kutatua migogoro pamoja na shughuli za kujenga amani, huku viongozi wakikubaliana kuwa mchango wa wanawake ni muhimu katika kuleta utulivu na maendeleo endelevu ya jamii.

Kupitia ushiriki wake katika mkutano huo, Tanzania imepata fursa ya kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa utakaosaidia kuendeleza ajenda za usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na maendeleo ya jamii kwa manufaa ya wananchi wake.

Hakuna maoni: