Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) limeeleza kuridhishwa na Bajeti ya Taifa ya mwaka wa fedha 2026/27, likisema kuwa itachangia kuimarisha mazingira ya biashara, kuvutia uwekezaji na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi nchini.
Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha wadau wa sekta binafsi jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sera, Utafiti na Utetezi wa TPSF, Bi. Mwanahamisi Hussein, amesema sehemu kubwa ya bajeti hiyo imezingatia maoni na mapendekezo yaliyowasilishwa na shirikisho hilo kwa Serikali.
Bi. Mwanahamisi ameeleza kuwa hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kujenga uchumi imara na unaojumuisha wadau wote muhimu wa maendeleo.
Aidha, TPSF imepongeza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali kupitia bajeti hiyo, ikiwemo kuongeza tozo kwa baadhi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, hatua inayolenga kulinda wazalishaji wa ndani na kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mkutano huo wamebainisha kuwa bajeti ya mwaka 2026/27 imezingatia mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kutoa ushauri na mapendekezo yatakayochochea maendeleo ya taifa.
Ikumbukwe kuwa tarehe 11 Juni 2026, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, aliwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/27. Katika hotuba yake, Waziri huyo alisema Serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 62.33, sawa na ongezeko la asilimia 10.3 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni