Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, Juni 10, 2026 amepokea taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa Malagarasi kutoka kwa timu ya wakaguzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kufuatilia maendeleo ya miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta ya nishati.
Taarifa hiyo imewasilishwa katika kikao kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. Kikao hicho kilihudhuriwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Petro Lyatuu, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.
Hatua ya kupokea taarifa hiyo inafuatia ziara ya Waziri Ndejembi aliyofanya Mei 10, 2026 katika Mradi wa Umeme wa Malagarasi uliopo mkoani Kigoma, ambapo alieleza kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 49.5 za umeme kupitia maporomoko ya Mto Malagarasi.
Waziri huyo alibainisha kuwa kulikuwa na ucheleweshaji wa baadhi ya shughuli za ujenzi pamoja na kutotekelezwa kwa baadhi ya masharti ya mkataba kati ya TANESCO na kampuni ya Dongfang inayotekeleza mradi huo.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Ndejembi aliielekeza TANESCO kufanya ukaguzi wa kina wa mradi huo na kuwasilisha taarifa ya tathmini ili Serikali iweze kuchukua hatua stahiki za kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma ya umeme kwa wananchi kama ilivyopangwa.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni