Breaking


Jumanne, 14 Julai 2026

LAMINE YAMAL: “SINA HOFU, HUU NDIYO MCHEZO MUHIMU ZAIDI KWANGU”

 

Nyota wa timu ya taifa ya Hispania, Lamine Yamal, amesema yuko tayari kwa changamoto ya nusu fainali ya Kombe la Dunia 2026, akisisitiza kuwa hana hofu licha ya kukiri kuwa huo ndio mchezo muhimu zaidi kuwahi kuucheza katika maisha yake ya soka.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya mchezo huo mkubwa, Yamal alisema ana imani na uwezo wake na hataruhusu presha ya mechi kumzuia kuonyesha kiwango chake bora.

“Niko tayari kwa changamoto. Huu ndio mchezo muhimu zaidi ambao nimewahi kuucheza katika maisha yangu ya soka hadi sasa. Lakini sina hofu,” alisema Yamal.

Mchezaji huyo mwenye umri mdogo pia alizungumzia maoni yanayotolewa kuhusu kiwango chake cha uchezaji, akisema hafungwi na matarajio ya watu bali anaendelea kujiamini.

“Watu wengi wanasema sipo kwenye kiwango changu bora, hivyo naamini hawatarajii mengi kutoka kwangu kesho. Tayari najua kesho itakuwa siku ya kipekee kwangu.”

Yamal alieleza kuwa kikosi cha Hispania kinaamini kina uwezo wa kutwaa ubingwa wa dunia, akirejea mafanikio ya taifa hilo mwaka 2010.

“Bila shaka tunajiona tunaweza kuwa mabingwa wa dunia, kama ilivyokuwa mwaka 2010. Kwa nini isiwezekane? Tunaamini tunaweza kufanya hivyo.”

Kuhusu presha ya mechi kubwa, mshambuliaji huyo alisema anachofanya ni kucheza soka kwa uwezo wake wa kawaida bila kujipa mzigo wa ziada.

“Hakuna presha. Nacheza kwa namna ninavyojua. Sitacheza vizuri zaidi au vibaya zaidi ya uwezo wangu. Ukitoa kila kitu ulichonacho na watu wakaona juhudi zako, hutahisi presha.”

Akizungumzia suala la kufunga mabao, Yamal alisema si jambo linalomsumbua, ingawa anatambua kuwa kufunga katika mechi kubwa kama hiyo ni jambo la kipekee.

“Mabao hayanipi wasiwasi, lakini kufunga katika mechi kama hizi huwa ni jambo maalum. Ninalikubali hilo.”

Hispania inatarajiwa kushuka dimbani dhidi ya Ufaransa katika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2026, huku macho ya mashabiki wengi yakielekezwa kwa Lamine Yamal, ambaye ameendelea kuwa mmoja wa wachezaji wanaovutia zaidi katika mashindano hayo kutokana na kiwango chake na kujiamini akiwa bado na umri mdogo.


Hakuna maoni: