Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Dkt. Revocatus Mushumbusi, amepongeza taasisi na idara zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kama jukwaa la kutoa elimu, huduma na kuonesha fursa mbalimbali zinazowanufaisha wadau na wananchi.
Dkt. Mushumbusi amesema hayo Julai 13, 2026, alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii akiwa ameambatana na Meneja Rasilimali Watu na Utawala, Bi. Genofeva Shirima katika siku ya Kilele cha Maonesho hayo yanayofanyika katika Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, ametembelea mabanda ya taasisi na idara mbalimbali zinazoshiriki maonesho hayo kwa lengo la kujionea huduma zinazotolewa, kupata taarifa kuhusu shughuli zinazotekelezwa na kutambua fursa zinazotolewa kwa wadau na wananchi kupitia sekta za misitu, nyuki, utalii, wanyamapori, malikale na maeneo mengine yaliyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Dkt. Mushumbusi amepongeza juhudi za taasisi na idara hizo katika kuwasogezea wananchi huduma na elimu kupitia maonesho hayo, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutumia mbinu bunifu katika utoaji wa huduma ili kuongeza uelewa wa wananchi.
Akiwa katika banda la TAFORI, Dkt. Mushumbusi pia amehimiza taasisi kuendelea kuimarisha usambazaji wa matokeo ya tafiti kwa kutumia mbinu bunifu na huduma za kitaalamu, ili kuhakikisha wadau wa sekta ya misitu na nyuki wanapata taarifa sahihi na zenye manufaa kwa maendeleo ya sekta hiyo.
Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yalianza Juni 28, 2026 na yanahitimishwa leo Julai 13, 2026 katika Viwanja vya Sabasaba, Jijini Dar es Salaam.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni