Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa hali ya hewa kwa saa 24 zijazo kuanzia saa 3:00 usiku wa Julai 23, 2026, ikieleza kuwa maeneo mbalimbali nchini yanatarajiwa kuwa na mchanganyiko wa mawingu, vipindi vya jua pamoja na mvua katika baadhi ya maeneo.
Kwa mujibu wa utabiri huo, mikoa ya Kagera na Mara inatarajiwa kuwa na hali ya mawingu kiasi, huku mvua zikiambatana na ngurumo zikitarajiwa kunyesha katika maeneo machache, hasa wakati wa vipindi vya jioni.
Katika Visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani (ikiwemo Mafia), kunatarajiwa kuwa na hali ya mawingu kiasi pamoja na mvua nyepesi katika maeneo machache.
Kwa upande wa mikoa ya Dodoma, Singida, Kigoma, Tabora, Katavi, Morogoro, Lindi, Mtwara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu, Ruvuma, Mbeya, Rukwa, Iringa, Njombe na Songwe, hali ya hewa inatarajiwa kuwa na mawingu kiasi na vipindi vya jua katika maeneo mengi.
TMA imewataka wananchi kuendelea kufuatilia utabiri wa hali ya hewa na tahadhari zinazotolewa mara kwa mara ili kupanga shughuli zao za kila siku kwa kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa. Aidha, taarifa hiyo imeambatana na viwango vya joto pamoja na muda wa mawio na machweo ya jua kwa baadhi ya miji nchini kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kupanga shughuli mbalimbali.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni