Breaking


Jumamosi, 18 Julai 2026

VIFURUSHI VYA PAMOJA, SARARI ZA NDEGE KUIMARISHA ONGEZEKO LA WATALII TANZANIA NA MISRI


SERIKALI ya Tanzania ipo tayari kuandaa Mpango wa Vifurushi vya Pamoja  kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini na Jamhuri ya Watu wa Misri  kwa lengo la kutanua soko la kuuza mazao ya utalii ili kusaidia ukuaji wa uchumi kupitia utalii baina ya mataifa hayo mawili.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) wakati akishiriki ufunguzi wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Misri lenye lengo la kufungua milango na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo kwenye uwekezaji wa viwanda na biashara zinazoweza kusaidia ukuaji wa uchumi wa taifa.

“Sisi tupo tayari kuandaa Mpango huu wa pamoja kwa nchi zetu zote mbili, lakini pili taasisi zetu ikiwemo Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), TANAPA, Ngorongoro na Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZCT) wapo tayari kuandaa mkakati huo mahsusi wa kuendeleza na kutangaza zaidi utalii wa kihistoria, kiutamaduni na dini,” amesema Mhe. Chande.

Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ikiwemo mbuga za wanyampori, Mlima Kilimanjaro, utalii wa urithi wa kihistoria na Dini kama inavyoelezwa na baadhi ya watafiti mbalimbali kuwa Dini ya Ukristo na Uislam kwa Afrika Mashariki zilianzia Bagamoyo, Kunduchi, Zanzibar pamoja na Kilwa iliyoanza kusimama na kujitengenezea sarafu yake yenyewe mwanzoni mwa karne ya 15.

"Wenzetu wa Misri wameendelea zaidi katika  utalii wa kihistoria kwa hiyo ili kufanikisha hili kwa pamoja, sisi tupo tayari kushirikiana katika eneo hili la kutangaza vivutio vya utalii kwenye vivutio vyetu na tutashukuru wenzetu wa Sekta ya Uchukuzi wakiendeleza ushirikiano wao kuimarisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na Misri ili watuletee wageni waone vivutio vyetu,” amesisitiza Mhe. Chande.

Hadi kufikia mwaka 2025/2026 Sekta ya Utalii nchini imekua na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na Pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 20 kutokana na ongezeko la wageni kutoka mataifa mbalimbali kutembelea vivutio vya utalii hivyo, kuanzishwa kwa Mpango huo wa Vifurushi vya Pamoja na safari za ndege kati ya Tanzania na Misri itasaidia kufikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais.  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufikia idadi ya watalii million 8 kufikia 2030.

Hakuna maoni: