Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Diwani Msemo, akiwa na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Computech Healthcare Solutions Hanif Popat, amejionea na kukagua mashine mpya ya tiba mionzi ya ELEKTA Harmony inayotoa huduma za matibabu ya saratani kwa kiwango cha kibingwa na ubingwa bobezi kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Mashine hiyo inatumia teknolojia za kisasa za Image Guided Radiotherapy (IGRT) zinazowezesha utoaji wa tiba ya mionzi kwa usahihi wa hali ya juu kwa kuzingatia eneo halisi la uvimbe. Pia Mashine hii hutumia mfumo wa kisasa wa kupanga na kutoa dozi ya mionzi kulingana na umbo na ukubwa wa uvimbe hivyo kulinda kwa kiwango kikubwa tishu na viungo vyenye afya vilivyo karibu na eneo linalotibiwa.
Aidha ina uwezo wa kutibu aina mbalimbali za saratani kwa kutumia mbinu za kibingwa na ubingwa bobezi, ikiwemo Volumetric Modulated Arc Therapy (VMAT), Intensity Modulated Radiotherapy (IMRT) na mbinu nyingine za kisasa zinazowezesha tiba kutolewa kwa usahihi mkubwa.
Kutokana na teknolojia yake ya hali ya juu, Elekta Harmony hupunguza muda ambao mgonjwa hutumia ndani ya chumba cha matibabu jambo linaloongeza faraja na utulivu wakati wa matibabu huku likiboresha ufanisi waj huduma na kuongeza idadi ya wagonjwa wanaoweza kuhudumiwa kwa siku.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni