Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye ukurasa wake rasmi wa Instagram leo, Jumapili, Zuchu amesema amefikia uamuzi huo baada ya miaka sita ya kuwa kwenye uhusiano, akieleza kuwa sasa ameamua kujipa kipaumbele.
“Hello my GPG, mimi na aliyekuwa mwenzangu we are now separated and going through a divorce,” aliandika Zuchu kwenye ujumbe wake.
Katika ujumbe huo, Zuchu amesema anamtakia kila la heri Diamond Platnumz pamoja na familia yake, huku akibainisha kuwa kipindi hiki anakusudia kuelekeza nguvu zake katika afya yake, uponaji wa kihisia na shughuli zake za kikazi.
“As for me muda huu ni wa kupona na kufocus zaidi kwenye afya na kazi zangu. Rizki imeisha, Alhamdulillah. Tulijaribu lakini Allah ana mipango yake na sina budi kuikubali,” ameandika.Tangazo hilo limeibua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wao kwenye mitandao ya kijamii, likifuatia kipindi ambacho kumekuwa na taarifa mbalimbali kuhusu mwenendo wa uhusiano wao.
Hata hivyo, ni muhimu kutambua kuwa wawili hao wamewahi kuripotiwa kutengana na baadaye kurejeana katika siku zilizopita. Kutokana na historia hiyo, haijafahamika kwa sasa ikiwa hatua hii itakuwa ya kudumu, kwani hakuna taarifa nyingine rasmi kutoka kwa Diamond Platnumz kuhusu tangazo hilo.
Zuchu na Diamond Platnumz ni miongoni mwa wasanii maarufu wa muziki wa Tanzania, na uhusiano wao umekuwa ukifuatiliwa kwa karibu na mashabiki kwa miaka kadhaa. Kufikia sasa, mashabiki wanaendelea kusubiri iwapo kutakuwa na tamko rasmi kutoka kwa Diamond Platnumz kuhusu suala hilo.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni