Jamii imehimizwa kuchukua tahadhari na kuzingatia afya ya mapafu na mfumo wa upumuaji ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa yanayoweza kuathiri uwezo wa mtu kupumua na kufanya shughuli zake za kila siku.
Magonjwa ya mfumo wa upumuaji yanaweza kusababishwa na sababu mbalimbali, ikiwemo maambukizi, moshi, vumbi, hewa chafu na mazingira yenye vihatarishi vya kiafya.
Dkt. Luth Mwapule Daktari Bingwa Bobezi wa Magonjwa ya Mapafu na Mfumo wa Upumuaji amewashauri wananchi kujikinga kwa kuepuka mazingira yenye moshi na vumbi, kuhakikisha hewa safi katika maeneo ya makazi na kazi, pamoja na kuzingatia usafi wa mikono na njia nyingine za kuzuia maambukizi.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwapule, mtu anayepata dalili zinazoendelea kama kukohoa kwa muda mrefu, kupumua kwa shida, maumivu ya kifua au homa anashauriwa kufika katika kituo cha afya kwa uchunguzi badala ya kujitibu bila ushauri wa mtaalamu.
Amesisitiza kuwa uelewa wa jamii kuhusu afya ya mapafu ni muhimu katika kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na magonjwa ya mfumo wa upumuaji ambapo wananchi wanapaswa pia kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya, kufuata hatua za kinga na kuwahi kupata huduma pale wanapohisi mabadiliko yasiyo ya kawaida katika mfumo wao wa upumuaji, hatua inayoweza kusaidia kubaini na kutibu tatizo mapema.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni