Maafisa wa ufuatiliaji na tathmini wa Wizara ya Fedha na Taasisi zilizo chini yake wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kuzingatia ushauri wa kitaalamu ikiwemo kuwasilisha taarifa kwa wakati ili kufanikisha madhumuni ya ufuatiliaji na tathmini na kuhakikisha mipango, programu na miradi ya Serikali inatekelezwa kwa ufanisi na kuwezesha kufikia matokeo yaliyotarajiwa na kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Fedha, Bi. Theresia Henjewele, wakati wa
Kufunga Jukwaa la Kwanza la Ufuatiliaji na Tathmini la Wizara ya Fedha kwa mwaka 2026/27, lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Cate Hotel mkoani Morogoro.
Alisema Jukwaa hilo limekuwa fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu na kupata mafunzo kutoka kwa wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuwajengea uwezo maafisa hao katika kufanya ufuatiliaji na tathmini ili matokeo yaweze kuisaidia Wizara kufanya maamuzi yenye ushahidi kama ilivyoelezwa kwenye kauli mbiu ya jukwaa hilo.
‘’Jukwaa hili limesaidia kujenga uelewa wa pamoja, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha ufuatiliaji na tathmini kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Fedha, hivyo ni vyema wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini wa wizara na taasisi zake mliopata mafunzo haya mkayatekeleze katika utendaji wenu’’ alisema Bi. Theresia Henjewele.
Aidha, alisema ufuatiliaji na tathmini ni sehemu muhimu katika kuhakikisha utekelezaji wa mipango na shughuli za Serikali unafanyika kwa ufanisi, huku taarifa zinazozalishwa zikisaidia katika kufanya maamuzi sahihi.
“Katika ufuatiliaji na tathmini, tunahitaji kukubaliana hatua za pamoja za kuendelea kuboresha na kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini,” alisema. Bi. Theresia Hanjewele.
Alisema ushirikiano wa viongozi na wataalamu kutoka kada mbalimbali wa taasisi ni muhimu katika kujenga mfumo imara wa ufuatiliaji na tathmini utakaowezesha Wizara kufuatilia maendeleo ya utekelezaji, kutambua changamoto kwa wakati na kuchukua hatua stahiki.
Kwa upande wa washiriki wa Jukwaa hilo hususan Maafisa wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Taasisi zote zilizopo chini ya Wizara wameipongeza Wizara ya Fedha, kwa kuandaa Jukwaa hilo na kuwapatia mafunzo kupitia mawasilisho mbalimbali ambayo yamewajengea uwezo katika eneo la ufuatiliaji na tathmini huku wakiiomba Wizara iendelee kuwajengea uwezo Maafisa wa Ufuatiliaji na Tathmini kupitia mafunzo na makongamano mbalimbali ili kuendelea kuboresha.
Jukwaa la Kwanza la Ufuatiliaji na Tathmini la Wizara ya Fedha kwa Mwaka 2026/27, lenye Kaulimbiu “Kuimarisha Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini kwa Maamuzi Yenye Ushahidi” limekuwa na wawezeshaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Msajili wa Hazina na Chama cha Wataalamu wa Tathmini Tanzania (TANEA).
Aidha, Jukwaa hilo liliwahusisha washiriki kutoka Wakuu wa Idara, Vitengo na Sehemu za Ufuatiliaji na Tathmini wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha, Maafisa Viungo wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na Maafisa wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Fedha.
Kupitia Jukwaa la Kwanza la Ufuatiliaji na Tathmini la Wizara ya Fedha kwa Mwaka 2026/27, Wataalamu wa Ufuatiliaji na Tathmini wamepata uelewa wa pamoja ambao utasaidia kuboresha namna ya kuandaa taarifa za ufuatiliaji na tathmini, kufanya uchambuzi wa matokeo na kutumika katika kuboresha utekelezaji wa majukumu ya taasisi.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni