Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeungana na wahifadhi wengine duniani kuadhimisha Siku ya Faru Duniani kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu uhifadhi wa faru na kutambua jitihada zinazofanywa na askari pamoja na wadau wa uhifadhi kumlinda Faru.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi NCAA, Naibu Kamishna wa Uhifadhi (Huduma za Shirika) Aidan Makala amesema maadhimisho ya Faru yanawaleta pamoja wadau wa uhifadhi na wenyeji wa Ngorongoro kuhamasishana umuhimu wa ulinzi na uhifadhi wa mnyama faru ambae ni alama muhimu ya kuvutia wageni Ngorongoro.
“uhifadhi wa faru unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Mamlaka, wadau wa uhifadhi na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi, tunashukuru kuwa jitihada za pamoja zimesaidia kuongeza idadi ya Faru ndani ya hifadhi na kuvutia watalii wengi ambao wanapokuja Ngorongoro ndio eneo pekee la kumuona Faru kwa karibu akiwa katika mazingira ya asili” alisema DCC Makala.
Kwa upande wake Albert Mollel, Mkurugenzi wa shirika la Naples Zoo Tanzania, amesema shirika hilo linalojiihusisha na uhifadhi litaendelea kushirikiana na NCAA kuhakikisha kuwa juhudi za uhifadhi zinakuwa endelevu na zenye manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Wadau waliohudhuria kwenye maadhimisho hayo ni pamoja na Friedkin Conservation Fund,
Naples Zoo, Labalaba, Nomad
and beyond na Tanzania people and Wildlife (TPW) ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “Keep the Five Alive”
Siku ya Faru Duniani huadhimishwa kila mwaka Septemba 22 kuhamasisha dunia kuhusu changamoto zinazowakabili faru na umuhimu wa kuchukua hatua za pamoja katika kuwalinda dhidi ya vitisho vinavyoweza kuhatarisha uwepo wao.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni