Leo Septemba 22, 2026, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, imetoa tamko kupitia Vyombo vya habari kuhusu matukio yaliyo sababisha vifo vya watumishi wa uhifadhi Mkoani Tabora na lile la vifo vya wanyamapori lililotokea katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro Mkoani Arusha.
Akitoa taarifa hiyo kwa umma katika mkutano na waandishi wa habari, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema tukio la kwanza lilitokea mnamo Septemba 18 2026 katika eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Ipole Wilayani Sikonge Mkoani Tabora wakati watumishi wa uhifadhi wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kulinda rasilimali za Taifa na kusababisha vifo vya watu 6 na majeruhi 5
Taarifa hiyo ya Waziri Kijaji imeeleza kuwa uchunguzi kuhusu chanzo, mazingira na wahusika wa tukio hilo unaendelea kufanywa na Jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama na hadi sasa watu 34 wanashikiliwa kwa ajili ya kusaidia uchunguzi.
Kuhusu tukio la vifo vya wanyamapori lililotokea katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, tarehe 18, Septemba 2026, Waziri Kijaji katika taarifa yake amesema hadi sasa vifo vilivyothibitishwa ni vya simba 11 na fisi 2 ambapo pia uchunguzi wa awali umebaini uwepo wa majeraha kwenye mizoga ya baadhi ya wanyamapori hao, hata hivyo uchunguzi zaidi bado unaendelea.
Dkt. Kijaji amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua zinazohitajika kuboresha mazingira ya utendaji kazi na usalama wa watumishi wanaotekeleza majukumu ya ulinzi wa rasilimali za Taifa, vilevile Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi kwa kuwa uhifadhi endelevu hauwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa wananchi wanaoishi jirani na maeneo hayo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mkazo katika Mawasiliano, ushirikishwaji wa jamii na utatuzi wa changamoto na migogoro inayojitokeza kwa njia za amani na kwa mujibu wa sheria.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni