Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeelekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kushirikiana na wadau pamoja na wawekezaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuwekeza kwenye vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo,Mhe. Timotheo Paul Mnzava (Mb.), wakati wa ziara maalum ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya utalii inayotekelezwa kwenye hifadhi ya Ziwa Duluti ikiwa ni dhamira ya Serikali kupitia Wizara, kuviendeleza na kuvitangaza vivutio vya utalii na kuwavutia wageni wakati huu ambao Tanzania inajiandaa na matukio mbalimbali ikiwemo Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027)
“Tutoe wito kwa wenzetu wa Serikali hasa Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kukaribisha na kuweka mazingira rafiki zaidi kwa wenzetu wa sekta binafsi ili watusaidie kuendelea kuboresha na kuongeza miundombinu ili maeneo yetu ya utalii yaendelee kuvutia lakini wageni wanapotembea waendelee kufurahia hasa katika kipindi hiki tunapojiandaa na AFCON” alisema Mhe. Mnzava.
Aidha, kamati hiyo imeipongeza Wizara kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuboresha miundombimu ndani ya hifadhi huku wajumbe wakielekeza kutumia vyema mitandao ya kijamii na watu maarufu kwa ajili ya kusaidia kutangaza kwa kasi Ziwa hilo la asili lililipo hapa nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb.) amesema kuwa Serikali itaendelea na mikakati mbalimbali ya kutangaza na kuuza maeneo mapya ya utalii ikiwemo Utalii wa dini uliopo kwenye hifadhi hiyo ili kutoa fursa kwa jamii kuendelea kufanya maombi na sala huku taifa likiendelea kunufaika na kujiongezea kipato kupitia fedha za kigeni kutokana na watalii kutoka ndani na nje ya nchi
Katika hatua nyingine Mhe. Chande amekaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuendelea kufanya uwekezaji katika Ziwa hilo ili kutanua wigo wa shughuli za utalii kutokana na yaliyomo kwenye Hifadhi hiyo ili kutoa fursa ya ajira kwa vijana waliopo hapa nchini na kujinufaisha kiuchumi
Aidha ametoa wito kwa watu mbalimbali kutembelea kivutio hicho cha asili katika kipindi hiki na kipindi cha Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON2027) ili kufurahia uzuri na upekee wa kivutio hicho chenye uwekezaji mkubwa wa eneo la malazi, utalii wa uvuvi, matembezi ya msituni, utalii wa utamaduni, dini, miamba na matembezi ya majini








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni