Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini-REA, imedhamiria kukamilisha miradi ya kusambaza umeme katika vitongoji vyote nchini ifikapo mwaka 2030, hatua ambayo itachochea shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Hassan Saidy, amesema hayo jijini Dodoma, wakati akizungumza katika Kikao Kazi cha Watumishi wa Wakala huo, kilichojadili utekelezaji wa majukumu, maendeleo ya miradi na kuimarisha usimamizi ili kuhakikisha malengo ya Wakala yanafikiwa kwa wakati.
Akisisitiza umuhimu wa wajibu walio nao watumishi katika kutekeleza dhamira ya Serikali ya kufikisha nishati vijijini, Saidy, amewataka kutambua kuwa mafanikio ya miradi yanagusa moja kwa moja maisha na shughuli za maendeleo za wananchi.
Aidha, amewataka wasimamizi wa miradi kutekeleza majukumu kwa weledi, uwajibikaji na uadilifu, sambamba na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi katika maeneo yao na kuhakikisha changamoto zinazoweza kuchelewesha miradi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Kupitia utekelezaji wa miradi hiyo, REA inaendelea kuimarisha juhudi za Serikali za kupanua wigo wa upatikanaji wa nishati vijijini, huku ikihimiza matumizi yenye tija ya umeme ili huduma hiyo iwe chachu ya kuinua uchumi wa wananchi na kuharakisha maendeleo katika maeneo ya vijijini.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni