Breaking


Jumatano, 23 Septemba 2026

TANZANIA YAPIGA HATUA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO, YASUKUMA MBELE AJENDA YA AFRIKA


Tanzania imetangaza azma yake ya kuwania nafasi ya uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2029–2030, huku ikiahidi kupeleka katika chombo hicho sauti imara ya Afrika na kusukuma mbele diplomasia ya kuzuia migogoro, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani na mageuzi ya operesheni za kulinda amani.

Msimamo huo umetolewa na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mjadala wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, unaofanyika jijini New York, Marekani.

Ndejembi amesema Tanzania ikichaguliwa itatoa kipaumbele kwa diplomasia ya kuzuia migogoro kabla haijawa vita, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani, kuimarisha nafasi ya wanawake katika ulinzi na ujenzi wa amani, kuongeza ushiriki wa vijana katika ajenda za amani na usalama, pamoja na kusukuma mbele mageuzi ya operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani.

Tanzania imesema dhamira hiyo imepata uungwaji mkono wa Umoja wa Afrika (AU), huku uchaguzi ukitarajiwa kufanyika Juni 2028.

Katika hotuba ya Makamu wa Rais, amesema, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kuongeza kiwango cha uzazi unaofanyika katika vituo vya afya kutoka asilimia 51 mwaka 2015 hadi asilimia 81 mwaka 2022. 

Amesema uzoefu katika hilo unaonyesha kuwa uwekezaji katika miradi inayotekelezeka na kuweka ustawi wa watu mbele, maendeleo yanaweza kuhama kutoka hatua ya ahadi hadi matokeo yanayoonekana na kupimika.

Tanzania pia imesisitiza umuhimu wa nchi zinazoendelea kupewa sauti kubwa zaidi katika taasisi na mifumo ya kimataifa inayofanya maamuzi ya kifedha yanayoathiri uchumi wake wa muda mrefu wa maendeleo, Tanzania imewasilisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kama msingi wa kujenga uchumi jumuishi, shindani na wenye uwezo wa kustahimili misukosuko, kupitia uwekezaji katika watu, miundombinu yenye tija, teknolojia, ubunifu, wanawake na vijana.

Aidha, Tanzania imeeleza mshikamano wake na Cuba, Zimbabwe na mataifa mengine yanayokabiliwa na vikwazo, huku ikitoa wito wa kuchukuliwa hatua za makusudi kuelekea kuondolewa kwa vikwazo bila masharti.

Kuhusu hali ya Gaza na Mashariki ya Kati, Tanzania inasisitiza umuhimu wa kuwalinda raia, kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia wanaohitaji bila vikwazo na kurejesha diplomasia kuwa njia kuu ya kutafuta amani ya kudumu.

Hakuna maoni: