Breaking


Jumatano, 23 Septemba 2026

WATU 11 WAUAWA KWA KUPIGWA RISASI NDANI YA NYUMBA AFRIKA KUSINI

Takriban watu 11 wameuawa kwa kupigwa risasi katika nyumba moja ya makazi karibu na jiji la Durban, nchini Afrika Kusini.

Polisi wamesema watu wenye silaha waliingia katika nyumba hiyo iliyoko katika mtaa wa KwaMakhutha na kuwafyatulia risasi watu 14.

Watu 10 waliuawa papo hapo, huku wengine wanne wakipelekwa hospitalini. Mmoja wao alifariki baadaye kutokana na majeraha, polisi wamesema.

Polisi wamesema baadhi ya waathiriwa walikuwa chini ya uangalizi wao kuhusiana na shughuli haramu, lakini hawakuweza kutoa maelezo zaidi kwa sasa ili kulinda uchunguzi unaoendelea.

Sababu ya shambulio hilo bado haijathibitishwa, ingawa polisi hawajapuuza uwezekano wa kuwa kulikuwa na mzozo kati ya makundi hasimu.

Afrika Kusini ina miongoni mwa viwango vya juu zaidi vya mauaji duniani. Takwimu za polisi zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 60 huuawa kila siku kwa wastani nchini humo.

Hakuna maoni: