Breaking


Jumapili, 27 Septemba 2026

MKURUGENZI MKUU WA SWISSPORT TANZANIA AIPONGEZA TCAA, AAHIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO



Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Dkt. Jabiri K. Bakari, Septemba 26, 2026 ametembelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Swissport Tanzania Plc, Bw. Joshua Jonas katika Ofisi za Makao Makuu ya TCAA, Banana, Ukonga, Dar es Salaam. Ziara hiyo ilitoa fursa kwa Bw. Jonas kujitambulisha kwa Mkurugenzi Mkuu na kujadili maeneo ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Swissport Tanzania, ambaye ni mtoa huduma za ardhini katika viwanja kadhaa vya ndege nchini na Mamlaka ambaye ni msimamizi wa sekta ya usafiri wa anga kwa ujumla.

Bw. Jonas alieleza kuthamini mchango unaoendelea kutolewa na TCAA katika kuwezesha na kuendeleza sekta ya usafiri wa anga nchini Tanzania. Alieleza kuwa Swissport Tanzania inaendelea kutoa huduma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), huku ikiendelea kuzingatia viwango vya juu vya huduma, usalama na uzingatiaji wa matakwa ya mamlaka za usafiri wa anga.

Aidha, Bw. Jonas alieleza kuwa Swissport Tanzania, ikiwa ni mwanachama wa IATA, hivi karibuni imekamilisha kwa mafanikio mchakato wa urejeshaji wa uanachama wake (recertification), hatua inayodhihirisha dhamira yake ya kuendelea kuzingatia viwango vinavyotakiwa katika sekta ya usafiri wa anga. Alisisitiza pia kuwa kampuni inaendelea kuwa na kiwango cha juu cha uzingatiaji wa matakwa ya TCAA na ina vibali na ithibati zinazohitajika kwa shughuli zake, kuanzia huduma za uwanjani (ground handling) hadi huduma nyingine za anga zilizoidhinishwa.

Kwa upande wake, Dkt. Bakari aliipongeza Swissport Tanzania kwa kuendelea kuzingatia matakwa na viwango vya usalama pamoja na utoaji wa huduma bora. Alimhakikishia Bw. Jonas kuwa TCAA itaendelea kuhakikisha waendeshaji wa huduma za anga wana vifaa, uwezo na taarifa zinazohitajika ili kukidhi mahitaji na mabadiliko yanayoendelea katika sekta hiyo.

Aidha, Dkt. Bakari alimweleza Bw. Jonas kuhusu uwepo wa Mfumo wa Huduma za Usafiri wa Anga (CASP) ambao sasa unatumika katika upatikanaji wa huduma za udhibiti na taratibu mbalimbali za kibiashara zinazohusiana na TCAA kwa njia ya kidijitali. Alisisitiza umuhimu wa Swissport Tanzania kutumia kikamilifu mfumo huo, ambao unalenga kurahisisha taratibu, kuongeza ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma. Mkurugenzi Mkuu alimtaarifu Mkuu huyo wa Swissport kwamba, sambamba na mapinduzi makubwa ya kimfumo kwenye Mamlaka, limeanzishwa Dawati la huduma kwa wateja (Helpdesk) huku akiwasihi Swissport kulitumia Dawati hilo kila wanapokabiliana na changamoto.

Dkt. Bakari aliongeza kuwa kuimarisha usimamizi wa taarifa na utoaji wa huduma kwa njia ya kidijitali ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayosisitiza matumizi ya teknolojia na mabadiliko ya kidijitali katika sekta mbalimbali.

Hakuna maoni: