Breaking


Alhamisi, 3 Septemba 2026

NEMC YATOA TAHADHARI KWA WATANZANIA KUELEKEA MVUA ZA EL NIÑO


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka Watanzania kuchukua tahadhari na kuimarisha utunzaji wa mazingira kuelekea kipindi cha mvua za El Niño, kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kaimu Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa NEMC, Bi. Martha Kawishe, amesema wananchi wanapaswa kuendelea kulinda mazingira katika kipindi hiki ambacho mvua zinatarajiwa, huku wakiepuka shughuli zinazoweza kuongeza hatari ya mafuriko.


Amesema utupaji holela wa taka, kuziba kwa mifereji, ujenzi katika njia za asili za maji na uharibifu wa maeneo oevu vinaweza kuongeza madhara wakati wa mvua kubwa. Aidha, maeneo ya mabondeni, kingo za mito, maeneo yenye miteremko pamoja na maeneo yenye mifumo duni ya kupitisha maji yanahitaji tahadhari zaidi.

Kawishe amesema NEMC imewataka wananchi kutotupa taka kwenye mifereji, mito na makorongo, huku Mamlaka za Serikali za Mitaa zikisisitizwa kuhakikisha njia za maji zinasafishwa na kubaki wazi ili kurahisisha mtiririko wa maji.

Aidha, NEMC imesisitiza umuhimu wa kulinda kingo za mito, mabonde na maeneo oevu, pamoja na kuchukua hatua za kuzuia mmomonyoko wa udongo ambao unaweza kuongeza athari za mvua kubwa.


NEMC pia imewataka waendelezaji wa miradi, viwanda, vituo vya mafuta, migodi, hospitali na maeneo yanayohifadhi kemikali au taka hatarishi kuhakikisha shughuli hizo zinasimamiwa kwa usalama. Hatua hiyo inalenga kuzuia vitu hivyo kusombwa na maji ya mafuriko na kusababisha uchafuzi wa vyanzo vya maji au kuhatarisha makazi ya wananchi.

Baraza limesema litaendelea kushirikiana na Serikali za Mitaa pamoja na taasisi nyingine katika kutoa elimu kwa wananchi, kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa mazingira, pamoja na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria dhidi ya shughuli zinazoharibu mazingira.

NEMC imewahimiza Watanzania kufuatilia taarifa rasmi zinazotolewa na TMA na kuchukua hatua za tahadhari mapema. Baraza limesisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ni hatua muhimu katika kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa na mafuriko.


Hakuna maoni: