Ubalozi wa Tanzania nchini Netherlands umeendelea kutumia diplomasia ya afya kama nyenzo muhimu ya kufungua milango ya ushirikiano kati ya Taasisi za afya za Tanzania, na zile za Nchini Netherlands, katika tafiti na elimu ya juu. Kupitia juhudi hizo, Ubalozi umeratibu kwa mafanikio ziara ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Nchini Netheralnds iliyoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Prof. Abel Makubi.
Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kupanua wigo wa ushirikiano wa kitaalamu na kibobezi wa muda mrefu katika maeneo ya huduma za kibingwa, mafunzo ya wataalamu wa afya, tafiti, ubadilishanaji uzoefu, teknolojia, na ubunifu ili kuboresha huduma za matibabu nchini Tanzania.
Kupitia ziara hii, BMH na Radboud University Medical Center (Radboud UMC) zimekubaliana kuanzisha ushirikiano kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalamu katika maeneo mbalimbali ya ubingwa bobezi wa matibabu.
Aidha, kupitia uratibu wa ZGT Overseas Foundation ya Netherlands, makubaliano yamefikiwa kati ya BMH na Amphia Hospital ya Breda-Netherlands, pamoja na Schüchtermann-Klinik – Heart Center, Bad Rothenfelde za Ujerumani, kuandaa mpango wa miaka mitano wa kupanua na kuimarisha huduma za kibobezi za moyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa. Mpango huo utatoa fursa za mafunzo ya juu, kubadilishana uzoefu na wataalamu wa kimataifa, pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za kisasa za kibobezi za moyo.
Katika kuimarisha ushirikiano wa afya kati ya Tanzania na Netherlands, BMH imedhamiria kuendelea kushirikiana na taasisi za ndani, zikiwemo JKCI, KCMC, BMC na Aga Khan, ili kutumia utaalamu uliopo kuimarisha huduma za moyo. Prof. Makubi amesisitiza kuwa ushirikiano huo ni kipaumbele cha BMH katika kukijenga kuwa kituo bora cha matibabu Afrika Mashariki.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni