Breaking


Jumamosi, 5 Septemba 2026

UN WAPIGA KURA KUHUSU RAMANI INAYOONYESHA UKUBWA HALISI WA AFRIKA


Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio linalolenga kuongeza uelewa kuhusu ukubwa halisi wa bara Afrika katika ramani za dunia, kufuatia mjadala kuhusu namna ramani za jadi zinavyowakilisha ukubwa wa mabara.

Azimio hilo, lililowasilishwa na Togo kwa kuungwa mkono na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), limepata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wanachama wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa kawaida halina nguvu ya kisheria ya kulazimisha nchi wanachama kubadilisha mifumo yao ya ramani.


Mjadala huo umejikita zaidi katika matumizi ya ramani ya Mercator, ambayo ilianzishwa mwaka 1569 na mchoraji ramani Gerardus Mercator. Ramani hiyo imekuwa maarufu kwa matumizi ya urambazaji, lakini inapotosha ukubwa wa maeneo kadiri yanavyokaribia ncha za dunia.

Kwa mfano, katika ramani ya Mercator, Greenland inaweza kuonekana kuwa na ukubwa unaokaribiana na Afrika, wakati kwa uhalisia Afrika ina eneo la takribani kilomita za mraba milioni 30.37, ikilinganishwa na takribani milioni 2.17 za Greenland.

Wataalamu wa ramani wanaeleza kuwa hakuna njia rahisi ya kuwakilisha uso wa dunia wenye umbo la duara kwenye karatasi ya pande mbili bila kuwepo kwa aina fulani ya upotoshaji. Ndiyo maana kuna aina mbalimbali za ramani zinazotumika kulingana na lengo, zikiwemo zile zinazolenga kuonyesha ukubwa wa maeneo kwa usahihi zaidi.


Hakuna maoni: