WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) umesema ujenzi wa miundombinu ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma umefikia asilimia 89, huku hatua za mwisho za kupata ithibati ya usalama wa anga zikiendelea kabla ya kuanza kwa matumizi rasmi ya uwanja huo.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema ujenzi wa miundombinu ya uwanja huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 27, 2026, wakati ujenzi wa majengo ukitarajiwa kukamilika Desemba 30, 2026. Amesema ujenzi wa majengo, unaojumuisha jengo la abiria, mnara wa kuongozea ndege, kituo cha kuzima moto, kituo cha umeme na huduma za hali ya hewa, umefikia asilimia 79.
Amesema pamoja na miundombinu kuwa katika hatua za juu za utekelezaji, kuanza kwa safari za ndege kutategemea kukamilika kwa taratibu za certification na kuchapishwa kwa taarifa rasmi za matumizi ya uwanja huo katika mifumo ya kimataifa ya usafiri wa anga. Amesema taratibu hizo zinalenga kuhakikisha uwanja unakidhi viwango vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), huku akieleza kuwa uwanja huo tayari umefanyiwa flight test.
Kwa mujibu wa Besta,Uwanja wa Msalato umejengwa kwa kiwango cha 4E cha ICAO, kinachouwezesha kuhudumia ndege kubwa na safari za ndani na kimataifa.
Amesema mradi huo una vifurushi viwili, ambapo kifurushi cha kwanza kinahusisha runway, taxiway, apron na barabara za mzunguko zenye thamani ya Sh bilioni 164.4, huku kifurushi cha pili kinachohusisha majengo kikigharimu Sh bilioni 195,na kwamba mradi umezalisha takribani ajira 9,000 kwa Watanzania.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni