Breaking


Alhamisi, 24 Septemba 2026

LATRA: SAFARI ZA USIKU ZIMEONGEZA UFANISI NA FURSA ZA BIASHARA


Uamuzi wa kuruhusu mabasi ya masafa marefu kufanya safari kwa saa 24 ni miongoni mwa mageuzi makubwa yaliyofanywa katika kuboresha huduma za usafiri wa barabara nchini.

Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini-LATRA, iliruhusu mabasi yaliyokidhi masharti kusafiri usiku na mchana, hatua iliyoongeza muda wa huduma kwa waendeshaji na kuwapa abiria fursa zaidi za kuchagua muda wa safari.


Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mkutano wa wahariri ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Dokta Habibu Suluo, amesema uamuzi huo uliwezekana kutokana na kuimarika kwa usalama, miundombinu ya barabara, mifumo ya mawasiliano pamoja na uwezo wa LATRA kufuatilia mabasi kupitia mfumo wa ufuatiliaji wa magari-VTS.


Tathmini zinaonesha kuwa huduma ya safari za usiku imechangia kupunguza ajali, msongamano katika vituo vya mabasi, huku pia ikipunguza ushindani wa baadhi ya madereva kuendesha kwa mwendokasi hatarishi ili kuwahi kufika wanakoelekea.

Aidha, abiria wengi wamekuwa wakipendelea kusafiri usiku kwa sababu huduma hiyo imepunguza au kuondoa hitaji la kugharamia malazi, hususan kwa wafanyabiashara wanaosafiri kati ya mikoa mbalimbali.

Kwa mujibu wa Dkt. Suluo, kuanza kwa safari za usiku kumeongeza fursa za biashara na uwekezaji katika sekta ya usafirishaji, pamoja na kuongeza ufanisi wa matumizi ya miundombinu ya barabara na ikiwemo kudhibiti uchovu wa madereva.

Hakuna maoni: